Dhana Ya Fonimu.

Fonimu
Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi,
fonimu ina maana, kwa kuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi katika
neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo
wa sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache ikilinganishwa na foni. Idadi
ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu
ishirini na nane (28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na
tatu (33) na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza kubadilishwa
nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa alofoni.
Alofoni ni kishio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa na
kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano:
• Fedha na feza
• Sasa na thatha
• Heri na kheri
Kwa kifupi, alofoni ni matamshi tofautitofauti ya fonimu [sauti] moja.
Mitazamo juu ya Dhana ya Fonimu.
Juhudi za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo
mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo
hujulikana zaidi.
(i) Fonimu ni tukio la kisaikolojia
Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni
Noam Chomsky. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhana iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha.Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa
bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake Chomsky anayaita maarifa haya kuwa ni
umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa
miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha
(kutamka) fonimu hizo, yaani utendi (performance). Chomsky anabainisha kuwa kuna
uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali
ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo
vya matamshi (alasauti za lugha), athari za mazingira, ulevi na maradhi. Hivyo kutoka na hali hii,
fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia tu.
(ii) Fonetiki ni tukio la kifonetiki
Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel James. Ambaye anaiona fonimu kuwa
ni {umbo} halisi linalojibainisha kwa sifa zake bainifu. Anadai kuwa fonimu huwakilisha
umbo halisi la kifonetiki na inapotokea kukawa na fungu la sauti katika fonimu moja, sauti
hizo huwa na sifa muhimu za kifonetiki zinazofanana. Hivyo, fonimu ya Kiswahili ni kitita
cha sauti za msingi pamoja na alofoni zake.
(iii) Fonimu ni Fonolojia.
Huu ni mtazamo wa kidhanifu, ambapo huaminika kuwa fonimu ni kipashio cha kimfumo, yaani
fonimu huwa na maana pale tuinapokuwa katika mfumo mahususi. Mwanzilishi wa mtazamo huu
ni Nikolai Trubetzkoy. Yeye huamini kuwa fonimu ni dhana ya kiuamilifu na uamilifu huu
hujitokeza tu fonimu husika inapokuwa katika mfumo wa sauti wa lugha husika. Kwa mujibu wa
mtazamo huu, fonimu ni kipashio kinachobainisha maana ya neno. Mtazamo huu hutumia jozi
sahihi kudhihirisha dai lake. Mathalani, maneno baba na bata yana maana tofauti kwa sababu ya
tofauti ya fonimu /b/ na /t/. Mtazamo huu hujulikana kuwa ni wa kifonolojia. Na kwa hakika,
mawazo haya ndiyo yaliyoshika mzizi zaidi katika taaluma ya fonolojia na ndiyo inayofunzwa
hivi sasa katika sehemu nyingi ulimwenguni.(Makala haya yaliandaliwa na ANTIDIUS JOVINARY NSIGA)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s