Riwaya za Kihistoria.

Riwaya za kihistoria ni tanzu za kimasimulizi ambazo huunda na kuitengeneza
historia kwa njia ya ubunifu. Ubunifu huu unajitokeza kupitia wahusika wa kubuni
au wahusika halisi ambao wameinuliwa kidogo katika namna ya utendaji wao
kuliko hali halisi. Pia, ubunifu huo unaweza kujitokeza kupitia utumiaji wa matukio
halisi ya kihistoria lakini yakaongezewa na wahusika wa kubuni pamoja na matukio
mengine yanayokusudia kuweka msisitizo wa ujenzi wa idili muhimu ya jamii kwa
kipindi hicho cha wakati (Mlaga, 2011; Gupta, 2007). Kundi hili la aina hizi za
riwaya katika fasihi ya Kiswahili limegawanyika katika makundi matatu. Msingi
wa mgawanyo huu ni kama ambavyo Tuner aliweka mgawanyo huu ili kukabiliana
na utata wa kubainisha sifa za riwaya za kihistoria. Makundi haya ya riwaya za
kihistoria ni pamoja na riwaya wazi (documented), riwaya fiche (disguised) na
riwaya za kubuni (invented). Aina hizi za riwaya za kihistoria zinafafanuliwa zaidi
moja baada ya nyingine katika mtiririko ufuatao:
Mosi ni riwaya wazi, hii ni aina ya riwaya ya kihistoria ambayo inatambulika kama
riwaya ya kihistoria hasa. Hii ni aina ya riwaya ya kihistoria inayojulikana kuwa ni
kongwe. Kimsingi aina hii ya riwaya ya kihistoria kwa sehemu kubwa hujitahidi
kuendana kwa ukaribu na vitabu vya historia. Katika aina hii ya riwaya mara nyingi
huhusisha watu na matukio halisi ya kihistoria. Pamoja na hivyo, riwaya za aina hii
huhakikisha msuko wake wa matukio ni wa kihistoria. Wahakiki wengi akiwemo
Mulokozi (1990) anaitazama aina hii ya riwaya kama ndio riwaya halisi ya
kihistoria.
Riwaya za aina hii zilifungamanishwa na falsafa kongwe ya historia ambayo
iliegemea katika imani juu ya ukweli mkamilifu, ukamilifu wa historia, usawiri wa
matukio kama yalivyotokea, kuitenganisha historia na ubunilizi, na kuikamilisha
historiografia ya kipindi husika. Sifa hizi zilikusudia kuitenganisha historia na
fasihi, jitihada hizi zilifanyika kuanzia mwishoni mwa karne ya kumi na nane kama tulivyobainisha.

Haikuwezekana kuitenga historia na fasihi kwa muda mrefu sana, kwani ilipofika
mwishoni mwa karne ya 19, ilionekana dhahiri kwamba vigezo vilivyowekwa
kuitofautisha historiografia na fasihi havitekelezeki (Braitenthaller, 2008).
Pamoja na hayo, aina hii ya riwaya ya kihistoria imekuwa na mabadiliko ya msingi.
Kwani kwa zama hizi si lazima sifa za riwaya wazi zote zijitokeze kwenye riwaya
zote za kihistoria. Riwaya ya kihistoria inaweza kuwa na sifa moja tu kati ya hizi
tulizozitaja. Mabadiliko haya, yamechochewa na mabadiliko ya falsafa ya historia
kutoka falsafa kongwe ya historia, mpaka falsafa ya historia ya zama hizi. Falsafa
hii mpya inaiangalia historia kama kitu kisichokuwa na ukweli mkamilifu, chenye
kubeba mapendeleo, kisichokuwa na ukweli wa aina moja, na kisichojitosheleza
kiushahidi. Katika makala haya, tumezingatia falsafa zote mbili za historia. Falsafa
hizi ni ile falsafa kongwe ya historia kwa upande mmoja, ambayo ndio msingi wa
riwaya kongwe za kihistoria , na kwa upande mwingine, ni falsafa ya historia za
zama hizi, ambayo kimsingi haiegemei katika kusisitiza usayansi wa historia na
jitihada za kutenganisha historia na fasihi.
Pili ni riwaya fiche (disguised), hizi ni riwaya za kihistoria ambazo hazihusishi
kwa uwazi matukio na watu halisi wa kihistoria. Licha ya kutobainisha wazi
matukio na watu halisi wa kihistoria, jambo linaloifanya aina hii ya riwaya
kuonekana kwamba ni ya kihistoria ni ushahidi wa kutosha ambao unamwonesha
mwandishi kuonesha shauku yake juu ya historia. Mwandishi huweza kuandika
historia fulani kwa ufiche ikiwa ni pamoja na kukwepa hali ya udhibiti kutoka
katika mamlaka. Kwa mfano, katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo kuna tukio
la kijana Tumaini kuamua kumpiga risasi mkuu wa wilaya kama hatua mojawapo
ya kuonesha kukerwa na namna ambavyo siasa ya Ujamaa ilivyoathiri maisha yake
kwa kumnyang’anya mali zake ambazo amezipata kwa tabu. Tukio kama hili
Wamitila (2003), analitafsiri kuwa ni tukio fiche la kihistoria linalorejelea historia
halisi ya Kupigwa kwa risasi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Kleruu na
mkulima aliyejulikana kwa jina la Mwamwindi. Tamthiliya ya Kaptula la Marx
nayo inaelezwa kubeba historia halisi kwa namna ya uficho. Riwaya za Shaaban
Robert kama vile Kufikirika na Kusadikika nazo zinaweza kutazamwa kama
zinazoeleza historia halisi ya kipindi cha ukoloni kwa namna ya uficho. Msingi wa
riwaya za namna hii ni pamoja na muktadha wa uandishi wake ambao husaidia
kubaini uhistoria katika riwaya inayohusika.
Tatu, ni riwaya ya kubuni (invented). Katika aina hii ya riwaya, wahusika na
matukio yanayosimuliwa yanakuwa ni ya kubuni tu. Kutokana na hali hiyo,
uhusiano wa mwandishi na kazi yake unakuwa ni kigezo muhimu sana katika kuifanya riwaya inayohusika kuwa ya kihistoria.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s