Mbinu za kusawiri wahusika.

Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mwandishi anaweza kutumia njia kadhaa na tofauti katika
kuwasawiri wahusika wake. Msanii ana uhuru sio tu wa kuwatumia wahusika wa aina fulani, bali
wa kuiteua namna ya kuwawasilisha wenyewe. Kama wasomi na wahakiki wa fasihi,
tunategemea sifa kadhaa kuwaelewa wahusika hao: maumbile yao, mienendo na tabia zao, lugha
zao, vionjo vyao, uhusiano wao na wahusika wengine, hisia zao kwao na wengine, mazingira na
mandhari yao, kiwango chao cha elimu, jamii yao nakadhalika.

Mbinu zinazotumika kusawiri wahusika ni kama vile; mbinu ya kimaelezi, mbinu ya kidrama,
mbinu ya uzungumzi nafsi wa ndani, mbinu ya majazi au matumizi ya majina, mbinu ya
kuwatumia wahusika wengine na mbinu ya ulinganuzi na usambamba.
Wamitila ameainisha na kuchambua mbinu zifuatazo ambazo hutumika katika kuwasawiri
wahusika. Mbinu hizo zimetolewa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Mbinu ya kimaelezi.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002:23-24), anayetumia mbinu hii huzieleza sifa za mhusika na
mara nyengine hutoa picha ya maneno inayomwelezea mhusika anayehusika. Kwa kutumia
mbinu hii, mwandishi anakuwa na nafasi ya kubainisha mapenzi au chuki yake dhidi ya
wahusika fulani. Hii ni njia rahisi ya kuwasawiri wahusika na hasa kwa kuwa mwandishi
anaweza kutoa maelezo machache yanayoifumbata tabia au wasifu wa mhusika ambao
ungechukua muda mrefu kutokana na matendo yake mwenyewe. Hata hivyo, hii ni mbinu
ambayo ina udhaifu pia.
Mbinu hii ya kimaelezi haimpi msomaji nafasi ya kushiriki katika kuitathmini tabia ya mhusia
fulani. Analazimika kuukubali msimamo na kuridhika na maelezo ya mwandishi. Mfano
unaofuata unaonesha namna ya mbinu hii inavyotumika; kutoka katika riwaya ya Vuta n`kuvute
ya Shafi A Shafi:
“Yasmini alikuwa na kijuso kidogo cha mdawiri mfano wa tungule na macho makubwa ambayo
kila wakati yalionekanwa kama yanalengwalengwa na machozi. Alikuwa na pua ndogo,
nyembamba na chini ya pua hiyo ilipangana midomo miwili mizuri iliyokuwa haitulii kwa tabia
yake ya kuchekacheka, huku akionyesha safu mbili ya meno yake mazuri. Alikuwa na kichaka
cha nywele nyeusi zilizokoza ambazo zilianguka kwa utulivu juu ya mabega yake. Alikuwa si
mrefu lakini hakuwa mfupi wa kuchusha, na matege aliyokuwa nayo yalizidi kuutia haiba
mwendo wake wakati anapotembea” (1999:1).

Haya ni maelezo ya mwandishi kumhusu mhusika huyu ambayo yanatokea katika sehemu ya
mwanzo. Ingawa hasemi wazi wazi, uteuzi wake wa maneno unatuelekeza kuamini kuwa ana
mtazamo fulani kumhusu mhusika na ambao huenda ukatuelekeza kwenye njia fulani.

Mbinu ya kidrama.
Wamitila (2002), mbinu hii ya ki-muhakati (ki-mimesia), kama ilivyo katika tamthilia,
huonyesha wasifu wa mhusika wake. Pia mbinu hii inamwezesha msomaji au mhakiki kumjua na
kumweleza mhusika bila ya kuathiriwa na mtazamo wa mwandishi au msimulizi kumhusu.

Mbinu ya uzungumzaji nafsi wa ndani.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mbinu hii hulinganuliwa na nyengine inayojulikana kama
mkondo wa king’amuzi/kirazini. Mawaazo yanayopatikana katika mbinu hii huwa na
mshikamano wa muwala, mawazo hayo yamepangika kama unavyoweza kutokea katika
ung’amuzi nafsi wa kawaida, yaani pale endapo mhusika anapoongea peke yake.
Kwa upande mwengine, mkondo wa king’amuzi ni mbinu inayotumiwa kuonyesha mawazo
hayo au hisia za wahusika bila ya kuyahariri mawazo hayo au kuyapanga kwa namna yoyote ile
iwayo. Hii ni mbinu inayotumiwa sana katika uandishi wa unaokita kwenye tapo la usasaleo.
Mbinu ya uzungumzi nafsi wa ndani hujulikana kama “mjadala wa ndani” au “mjadala mdogo”.
Mjadala unaonekana hapa unazihusisha sauti mbili zinazohusika kwenye majibizano. Sifa
muhimu ni kuwa lazima maswali au majibu yanayopatikana yaibuke katika sauti ambazo
zinawakalisha mikabala, imani au sifa tofauti.

Mbinu ya kuwatumia wahusika wengine.
Wamitila (2002:26), badala ya kuyatumia majina ya wahusika, mwandishi anaweza kusawiri
mhusika kupitia kwa kuelezwa na wahusika wengine. Wahusika wanaweza kuelezwa na
wahusika wengine, yaani tunawajua kutokana na maneno ya wahusika wenzao. Hapa pana
tathmini ya mhusika ambayo ni ya ndani (kwa wahusika wengine), kuliko ya nje kama ya
masimulizi (mbinu ya kimaelezi).
Hata hivyo lazima tukumbuke maneno anayoyatamka mhusika A kumhusu mhusika B yanaweza
kuangaliwa kwa njia mbili. Kwanza, yanaweza kutusaidia kumwelewa B kwa kutufichulia
mambo ambayo hatuwezi kuyajua bila ya kuelezwa. Pili, inawezekana kauli anazozitamka A
kumhusu B zikatuonesha alivyo mhusika A kuliko alivyo B.

Mbinu ya ulinganuzi na usambamba.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mwandishi anaweza kuitumia mbinu za usambamba na
ulinganuzi katika kuwasawiri na kuwakuza wahusika wake. Ulinganuzi ni nini? Huu ni
ulinganishi kwa kinyume. Kuweko kwa mhusika ambaye ni kinyume cha mhusika fulani huweza
kuwa ni mojawapo ya uhusika.
Mwandishi anaweza pia kuwaweka wahusika au kuwaonyesha kwa namna ambazo ni sambamba
na kwa njia hii humfanya msomaji au mhakiki aziwazie tofauti au mfanano wa sifa zao. Ni
muhimu kukumbuka kuwa ulinganuzi sio tu mbinu ya uhusika bali hutumiwa katika usimulizi
wa matukio na ukuzaji wa dhamira na maudhui.
Wakati huo huo mwandishi anaweza kuwasawiri wahusika kwa namna ambavyo tabia zao
zinaonesha kupingana kwa aina fulani. Yaani tukimwangalia mhusika kwa makini, tunahisi
kuwa kuna kupingana kwa sifa fulani katika uhusika wake. Hapa tunasema kuwa za ki-nzani.

Mbinu ya majazi au matumizi ya majina.

Wamitila (2002), waandishi wa kazi za kifasihi huweza kuyatumia majina ya wahusika ambayo
huakisi mandhari zao, wasifu wao, itikadi zao, vionjo vyao na kadhalika. Uchunguzi wa majina
ya wahusika lazima uhusishwe na msuko, mbinu za utunzi, ucheshi, dhamira na maudhui na
itikadi au motifu katika kaziinayohusika.
Tunapozungumzia kulandana kwa wahusika na majina yao katika kazi faulani ya fasihi, ni kule
kuwiana kwa matendo ya wahusika na majina yao, sifa zao na majina yao, lugha yao na majina
yao, kujiamini kwao na jinsi majina yao yalivyo, elimu yao na majina yao, maana ya majina yao
na jinsi yanavyofanana na wao wenyewe ambapo msanii wa kazi ya fasihi huzitumia sifa hizi,
katika kusadifu hali fulani iliyozoeleka katika jamii.
Maelezo hayo yalikuwa na mchango mkubwa kwa mtafiti katika kusukuma mbele utafiti huu.
Hii inatokana kuwa Wamitila ameweza kuonesha na kufafanua vipengele vya msingi ambavyo
vilitumiwa na mtafiti katika kuchambua lengo la utafiti na hatimae kuweza kufikia lengo la
utafiti huu.
Aidha, kamusi ya BAKIZA (2010:208), wamefasili neno kulandana kuwa, linatokana na nomino
landa lenye maana ya kitendo cha kufanana na mtu ama kushabihiana. Landana pia ni kitendo
cha mtu kuwa na sura inayofanana na mwenzake; shabihiana.
Ingawa maelezo ya BAKIZA juu ya neno kulandana hayakuelezwa kwa mkabala wa kifasihi,
hata hivyo, maelezo hayo yalitoa mwanga kwa mtafiti, kuhusu maana halisi ya neno kulandana,
ambapo aliitumia dhana hiyo katika uchambuzi wa data zake.
Wamitila (2002:64), sadifa katika fasihi; kwake yeye, sadifa ni uzuri au ubaya. Sadifa ni utukiaji
wa matukio kwa wakati mmoja na aghalabu kwa namna ya kushangaza inayoashiria bahati.
Umuhimu wa dhana hii unatokana na kujitokeza kwake kwingi katika kazi kadhaa za fasihi ya Kiswahili. Kwa kuanzia ni muhimu kutaja kuwa sadifa hutumiwa kama mbinu au kipengele cha
msuko au kimtindo. Katika baadhi ya tanzu, sadifa ni kipengele muhimu katika muundo wake.
Tuisomapo hadithi ya Jamaadar ya Mui huwa Mwema, yanayaona matumizi ya sadifa kuhusiana
na Kotini na wahusika wengine. Vivyo hivyo katika riwaya za M.S.Abdulla. Katika riwaya za
M.S.Abdulla huwa sadifa jinsi matukio ya wahalifu yanavyokunjuka na hatimaye kufichuka.
Sadifa katika kazi hizi ni kipengele cha lazima.
Maelezo haya ya Wamitila tunaona kuwa yana mnasaba na mshabihiano mkubwa katika mada
yetu ya kuchunguza dhana zilizobebwa na wahusika na zinavyolandana na majina yao, hivyo ni
dhahiri kwamba kupitia maelezo haya tuliyatumia kama dira ya kufikia lengo la utafiti wetu.
Njogu na Chimerah (1999), wameeleza kuhusu suala la sadifa kwa wahusika katika riwaya ya
Siku Njema, ambapo wahusika Bi Rahma kasadifu vyema, Rashid Omar kasadifu na anakufa
lakini kifo chake si cha kifasihi, Zawadi anasadifu kuolewa na Kongowe, mtoto wa miaka kumi
na sita, ilihali yeye ana miaka ishirini na mitatu na akiwa na elimu ya juu. Pia wahusika wengine
waliohakikiwa ni Alice MacDonald, Vumilia Abdalla, Amina na Juma Mukosi.
Ufafanuzi wa huu uliofanywa na Njogu na Chimerah unaonekana kuwiana vyema na mada yetu
hii ya kuchunguza dhana zilizobebwa na wahusika na zinavyolandana na majina yao, hivyo kwa
kuzingatia mbinu hii pia mtafiti alipata msaada mkubwa uliomwezesha kufikia malengo ya
utafiti wake.

(Makala haya yaliandaliwa na Mwalimu Omukabe wa Omukabe wa Chuo Kikuu cha Kenyatta

Idara ya Kiswahili)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s