Dhana Ya Wahusika.

Dhana ya wahusika katika kazi za fasihi imewahi kufasiliwa na watafiti kadhaa. Kama
ilivyokwishaelezwa kuwa wahusika katika kazi za fasihi ni viumbe wanaopatikana katika hadithi
yoyote ile. Viumbe hawa huwa sehemu ya kazi nzima. Pili, wahusika ni binaadamu
wanaopatikana katika kazi ya kifasihi, na ambao wana sifa za kimaadili, kitabia, kiitikadi,
kifalsafa ambazo hutambulishwa na wanayoyasema na wanayoyatenda. Wahusika huweza
kutambulishwa pia na maelezo ya mhusika au msimulizi, msingi wa hisia, hali ya kimaadili,
mazungumzo na matendo ya wahusika ndio kiini cha motisha au uhamasishaji wa wahusika
(Wamitila, 2002).
TUKI (1998:169), wamefasili wahusika kuwa ni watu, miti au viumbe vinavyowakilisha watu
katika kazi za fasihi. Wahusika hutumiwa katika kazi za fasihi ili kuwakilisha hali halisi ya
maisha ya watu katika jamii inayohusika. Katika mgogoro unaozungumziwa katika kazi ya fasihi
hutumiwa kuwakilisha mawazo mbalimbali ya pande mbili au zaidi za mgogoro huo.
Maelezo hayo ya Wamitila na TUKI yalikuwa na umuhimu mkubwa katika kusukuma mbele
kazi hii. Hii ni kutokana na kwamba, Wamitila amedokeza maswala muhimu sana katika kutoa
maana ya wahusika katika kazi za fasihi. Sifa kama zile za kimaadili, kitabia, kiitikadi, kifalsafa
ambazo huwa zinawatambulisha wahusika hao zilitupa mwanga na muongozo mzuri katika
utafiti wetu huu uliolenga kuchunguza namna wahusika wanavyolandana na majina yao katika
riwaya teuliwa.
Rono (2013) akimnukuu Msokile (1992:42-43), anaeleza kwamba, wahusika husawiriwa kisanaa
na mwandishi ili waweze kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha katika jamii. Mwandishi
huwasawiri wahusika kwa wasomaji wake kwa kutumia sifa pambanuzi walizonazo, jinsi
walivyo, mambo gani hawayapendi na yapi wanayapenda katika maisha yao na kadhalika.
Wahusika hao hutumia misemo, nahau, tamathali za usemi na methali katika mazungumzo yao
ili kujenga tabia na hali ya kisanaa Rono (ameshatajwa), anaendelea kueleza kuwa, wahusika wa kazi za sanaa huwa na tabia
zinazotofautiana kati yao kwa sababu mbalimbali. Kwanza kabisa inategemea mwandishi ana
lengo gani analotaka kuonyesha katika kazi yake ya sanaa. Pili, aina ya kazi ya sanaa inaweza
kuathiri aina ya wahusika jinsi walivyosawiriwa, kuaminika kwao, wanavyohusiana wao kwa
wao, uwakilishi wao na majina yao. Wahusika katika hadithi ni mhimili mkubwa katika fasihi
andishi na hata simulizi.
Aidha, Msokile (1992), akiwanukuu Penina Muhando na Ndyanao Balisdya wanasema kwamba
wahusika wanaweza kuumbwa kinafsia, kiakili na kimwili. Kutokana na ujenzi wa aina hii,
mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au anaweza kuonyesha mabadiliko yake kila
anapokutana na mazingira tofauti. Ataonyesha mabadiliko katika uhalisia wake kwa kuzingatia
nguvu zinazomzunguka kama vile za utamaduni, siasa, uchumi na kadhalika.
Kwa mujibu wa Wamitila (2008:369), wahusika ni nyenzo kuu katika fasihi kwa sababu
wahusika ndiyo dira ya matukio na matendo yanayopatikana katika kazi ya kifasihi inayohusika.
Mtazamo wa dhana ya wahusika hutofautiana kutegemea mkabala anaouchukua mhakiki na
nadharia ya fasihi inayohusika.
Mhusika ni mtendaji katika kazi ya kifasihi na huwa kielelezo cha viumbe wanaopatikana
ulimwenguni, ingawa si lazima sifa zote za mhusika zifungamane moja kwa moja na za
wanadamu. Hii ndio maana neno “mhusika” linatumika bali si ‘mtu’ au ‘Kiumbe’. Mwelekeo wa
kuwahusisha wahusika wa kifasihi na binadamu wanaopatikana katika hali halisi huathiri kwa
kiasi fulani matarajio ya usawiri wa uhusika. Upo mwelekeo mkubwa wa kuwachunguza
wahusika wa kifasihi kwa kuwafungamanisha na binadamu halisi na hata, labda kutokana na
athari za mielekeo ya kimaadili, tukitarajia kuwa wahusika, hasa wale wakuu watakuwa na
maadili fulani.

Hata hivyo, tunakubaliana na Kundera (2007) kuwa, wahusika wa kifasihi hawahitaji kupendwa
kutokana na maadili yao bali wanachotakiwa kufanywa ni kueleweka. Matendo yanayopatikana
katika kazi ya kifasihi huhusishwa na wahusika. Matendo hayo ni nguzo kuu ya dhamira na
maudhui yanavyoendelezwa katika kazi inayohusika. Mawazo hayo ya Kundera yalitupa
mwanga mkubwa wakati wa kuwachungua wahusika na namna wanavyolandana na majina yao
na namna walivyobebeshwa dhamira na waandishi wa riwaya teuliwa.
Kulingana na Njogu na Chimerah (1999:45), wahusika ni viumbe wa sanaa wanaobuniwa
kutokana na mazingira ya msanii. Mazingira haya yaweza kuwa ya kijiografia, kihistoria,
kijamii, kitamaduni au ya kisiasa. Wahusika hujadiliwa kwa namna wanavyoingiliana na
dhamira na hili hujitokeza kutokana na maneno, tabia na matendo yao, yaani kulingana na hulka
yao. Wahusika wa aina yoyote wawe watu au viumbe hurejelea na huakisi sifa na tabia za
binadamu katika jamii husika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s