Sifa za lugha tandawazi.

Kimsingi, kuna sifa bainifu moja katika lugha tandawazi ambayo ni ‘ufupishaji’. Ufupishaji
huu unatokea kutokana na ‘udondoshaji’, ‘unambaishaji’ na ‘umatamshi’. Sifa hizi ingawa
zinaweza kuangaliwa kama zinazojitegemea, ni vijitawi tu vya sifa moja kuu yaani ufupishaji.
Kama nitakavyoonesha hivi punde, lengo la sifa hizi tatu: ‘udondoshaji’, ‘unambaishaji’ na
‘umatamshi’ hulenga kufupisha neno, sentensi au kifungu cha sentensi ili mhusika aweze
kutuma maneno mengi iwezekanavyo kwa kutumia nafasi ndogo. Kwa maneno mengine
anafanya mawasiliano ‘marefu’ kwa kutumia maneno machache. Sifa hizi zimeelezwa kwa
undani na wataalamu kama vile Crystal (2001, 2004, 2008a, 2008b). Inawezekana kadri
utafiti katika eneo hili unavyozidi kuongezeka, ndivyo tutakavyogundua sifa bainifu nyingine
zaidi ya hii ya ufupishaji, na hata kupata mawazo mapya kutokana na tafiti hizo.
Sifa hii ya ufupishaji ni matokeo ya utandawazi. Utandawazi umefafanuliwa na watu
mbalimbali kwa mitazamo tofauti. Katika makala hii ninatumia neno ‘utandawazi’
nikikubaliana na Sullivan na Kymlick (2007: 1) waliofafanua kuwa:
Kuongezeka kwa maingiliano ya watu nje ya mipaka ya mataifa yao, hususan
katika nyanja za biashara na uwekezaji, lakini pia ni utoaji wa teknolojia, safari za
watu na mtawanyiko wa mitindo ya maisha ya kimagharibi inayosukumwa
ulimwenguni kupitia bidhaa kama vile sinema na filamu za Hollywood na vyakula
vya McDonald (Tafsiri ya mwandishi)
Katika maana hii ya Sullivan na Kymlick, suala la utolewaji wa teknolojia halijawa wazi
kama hayo mengine. Nchi nyingi zinazoongea Kiswahili kwa mfano, zimepokea zaidi bidhaa
zilizokwisha kuundwa kuliko zilivyopokea teknolojia. Kwa mfano, nchi hizi zimepokea simu
za kiganjani bila kupokea teknolojia ya utengenezaji simu hizo. Aidha, watumiaji wa simu
wamepokea simu hizo pamoja na namna fulani ya utamaduni katika matumizi ya simu.
Matumizi ya lugha ya mawasiliano katika simu hizi yamekuwa yakifanana kwa watumiaji wa
lugha ya Kiswahili mahali pengi wanapokuwa. Lugha hii tandawazi ina sifa kama
nilivyozieleza na inasukumwa mbele na utandawazi kama nilivyoueleza. Hata hivyo kuna sifa
ya ziada katika utandawazi popote ulimwenguni. Sifa hiyo ni watu kutaka kutumia zaidi huku
wakilipia kidogo. Sifa hii ndiyo tunayoiona katika matumizi ya simu: watumiaji wanataka
kuwa na maneno mengi kadri inavyowezekana, lakini wana nafasi ndogo katika simu zao, na wangelipenda kutokutumia fedha zaidi kama ikiwezekana. Ufupishaji wa mawasiliano
unaoletwa na lugha tandawazi unaweza kuonekana kuwa unamwelekeo huu.
Ikiwa tunakubaliana kuhusu sifa hii bainifu na vijitawi vyake, tutafakari sasa changamoto
zinazotolewa na lugha hii, katika nadharia za isimujamii. Nadharia tunayoijadili hapa ni ile
inayohusiana na kuchanganya msimbo na kubadili msimbo (code mixing na code switching).
Katika isimujamii, mbinu hii ya matumizi ya lugha hutokeza hali mbili ambazo zote uhusisha
maneno. Kwa mujibu wa King’ei (keshatajwa) kuchanganya msimbo hutokea pale ambapo
mzungumzaji huamua kuwa na misimbo au ‘ndimi’ zaidi ya moja katika usemi mmoja.
King’ei ametumia mifano ya misimbo ya Kiswahili na Kiingereza. Aidha ameelezea kuwa
mazingira ya uchanganyaji misimbo unaweza kuhusiaha lahaja za lugha moja, na hapo
amaonesha mifano ya uchanganyaji misimbo inayohusisha Kiswahili, Kiingereza na Sheng
(2010: 25). Katika mifano yote miwili, amefafanua uchanganyaji huo unaohusisha maneno tu.
Kubadili msimbo kunaelezwa kuwa ni “kuchanganya lugha mbili tofauti lakini katika kauli
tofauti badala ya kuwa katika usemi mmoja” (kama hapa juu). Na hata katika mfano huu,
maelezo yake yanahusisha maneno tu. Jambo hili ni tofauti katika lugha tandawazi; lugha
inayoletwa na matumizi ya simu za viganjani, barua pepe na maongezi katika tovuti. Utafiti
wa Crystal katika lugha hii ya simu za viganjani, umehusisha lugha ya Kiingereza tu. Ingawa
vitabu na makala zake zimesaidia sana kutoa mwanga katika makala hii, hazikujadili
changamoto zinazojitokeza kama lugha mbili au zaidi zikiwa pamoja. Mifano inayotolewa
toka kwa wazungumzaji wa Kiswahili na lugha nyingine ni ya kipekee ambayo hatuna budi
kuijadili kwa kina kama sehemu inayofuata inavyoanzisha mjadala huu.

(Makala haya ni kwa hisani ya Prof.Aldin Mutembei)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s