Utandawazi na mawanda ya matumizi ya simu.

Utandawazi na Mawanda ya matumizi ya simu
Jamii nyingi za Kitanzania kama zilivyo nyingi katika Afrika, bado zinaishi vijijini ambako
hakuna umeme. Aidha katika vijiji kama hivyo, hakukuwa na mawasiliano ya ‘simu za
mezani’. Kwahiyo, ilikuwa haiyumkiniki kuwa na mawasiliano kwa njia rahisi bila kuwepo
kwa miundombinu hasa umeme na simu. Upatikanaji wa simu za viganjani, na kukua kwa
matumizi yake kumeleta mabadiliko makubwa na kurahisisha mawasiliano. Matumizi ya
simu hizi mijini na vijijini ni mojawapo ya matokeo chanya ya utandawazi.
Simu hizi za viganjani zinatumika kwa wingi miongoni mwa wanajamii bila kujali umri,
jinsia, elimu au mahali mtu atokako. Wanajamii hawa huwasiliana kwa hutumia ‘lugha
tandawazi’, yaani lugha ya maandishi iliyochanganywa na namba huku ikifupishwa na
pengine kuchanganywa zaidi ya lugha mbili tofauti. Kutokana na ukweli huu swali letu la
kwanza ni je lugha tandawazi inayotumika katika mawasiliano ya simu inatumiwa na nani
hasa katika jamii? Je inatumiwa na wote (kama walivyotajwa hapa juu) au matumizi yake
yanajipambanua kutokana na umri, jinsia, elimu au mahali pa watumiaji? Swali jingine ni je,
tunaweza kuwa na sheria za lugha hii katika mawasiliano? Je mawasiliano haya yanaingia
katika mundo wa isimujamii uliokwisha kuwapo au yanaanzisha muundo mpya? Maswali
yote haya yanahitaji utafiti wa kina wa uwandani ili kuweza kujibiwa kiuyakinifu; makala hii
ni ya kiuchokozi kuanzisha mjadala kama huo.
Utafiti wa awali wa watumiaji wa lugha tandawazi kwa jiji la Dar es Salaam (Mutembei
2010), ulihusisha vijana wenye umri wa kati ya miaka 14 na 18 toka shule za Jangwani,
Azania, Tambaza, Makongo, Jitegemee na Mbezi. Mawasiliano ya vijana hao wa shule
yalilinganishwa na mawasiliano ya wafanyakazi wenye umri kati ya miaka 40 na 55 ambao
walichaguliwa toka Ofisi mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ardhi,
Chuo Kikuu kishiriki cha Chang’ombe na Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba – Muhimbili.
Sehemu zote mbili, ile ya shuleni na ile ya Vyuoni zilifanana kwa kuwa zote ni sehemu za
utoaji elimu. Wote walichukuliwa kuwa ni watu wenye uelewa na wanajitahidi kwenda na
wakati wakiathiriwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Katika utafiti huo, tuligundua kuwa wengi wa watumaji wa lugha tandawazi ni vijana
kutoka shule za sekondari. Katika jumla ya vijana 60 ambao walikubali kutupatia
mawasiliano mbalimbali waliyoyafanya na vijana wenzao, ni kijana 1 tu ambaye hakuwa na
wingi wa mchanganyiko wa namba, maneno, ufupishaji na mchanganyiko wa lugha mbili hasa za namba. Na kati ya wafanyakazi 60 ambao walikubali mawasiliano yao yaangaliwe
kama data ya utafiti, ni 4 tu ambao walikuwa wamechanganya namba, maneno na ufupishaji,
lakini hata hawa hawakuchanganya lugha mbili.
Bila shaka utafiti kama huo ukiweza kufanyika ukihusisha watu wengi zaidi na wa kada
mbalimbali unaweza kutupa majibu sio tu kuhusiana na vipengele vya isimujamii, bali hata
athari za lugha tandawazi hasa kwa mustakabali wa lugha ya Kiswahili. Ni kweli kwamba
kuenea kwa simu mahali pengi na kuongezeka kwa matumizi yake kumerahisisha sana
mawasiliano. Aidha ni kweli kuwa matumizi hayo yanakuza Kiswahili – lugha inayotumika
katika mawasiliano hayo. Tukiukubali ukweli huu, hatuna budi pia kuuangalia ukweli
mwingine unaojitokeza. Matumizi ya lugha tandawazi kwa njia ya simu na barua pepe
yanaweza kuwa na athari kubwa katika lugha ya Kiswahili nje ya miktadha ya mawasiliano
haya ya simu na barua pepe. Kabla hatujaangalia athari za lugha tandawazi nje ya wigo wa
simu na barua pepe, napendekeza tukubaliane kuhusu muundo wa mabadiliko ya kiisimujamii
katika lugha.
(Makala haya ni kwa hisani ya Prof.Aldin Mutembei)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s