Utandawazishaji wa Kiswahili kupitia simu.

Mojawapo ya matokeo ya utandawazi ni kuwapo kwa simu za kiganjani1 na matumizi yake.
Siku hizi nchini Tanzania mawasiliano ya simu yamekuwako kwa wingi kuliko ilivyokuwa
tangu wakati wa uhuru hadi katikati ya miaka ya tisini. Mahali ambapo hakukuwa na
mawasiliano kabisa, kama sehemu nyingi za vijiji vya Tanzania, siku hizi kuna mawasiliano
kwa njia ya simu hizi za kiganjani na lugha inayotumika katika mawasiliano haya ni
Kiswahili. Lugha ya Kiswahili inayotumika katika simu hizi ni ya kiutandawazi na pengine si
rahisi kuiona nje ya wigo huu wa kiutandawazi ambao pia unajumuisha mawasiliano kwa
barua pepe, na maongezi katika tovuti. Katika lugha hii ya kiutandawazi, watu huwasiliana
kwa kutumiana matini fupi fupi zenye mchanganyiko wa maneno na namba, na hivyo kuunda
lugha tofauti na iliyozoeleka katika jamii nyingine.Mbali na lugha hii katika simu, barua pepe, na Tovuti, Kiswahili kimeshuhudia pia
matumizi ya Sheng hasa miongoni mwa vijana. Lugha hii ipo kwa wingi nchini Kenya
ambapo wataalamu wa isimu na lugha wamekwisha kuiandikia Kamusi (Mbaabu 2003), na
hata makala (Mokaya 2006; Momanyi 2009). Lugha hii pia inatumika hasa katika programu-
pendwa za vijana katika stesheni za radio na TV katika Afrika mashariki. Ingawa lugha kamaSheng imefanyiwa utafiti na imeandikwa, lugha hii ya kiutandawazi inayojichomoza sasa
kupitia katika barua pepe, simu za kiganjani na maongezi katika Tovuti, bado haijavuta – kwa
kiasi kikubwa, shauku ya wataalamu na wapenzi wa lugha hata kuifanyia utafiti. Makala
chache kuhusu suala hili zimeongelea lugha hii katika mawanda tofauti. Kwa mfano, Butts na
Cockburn (2001) wameandika wakitathmini utumaji wa matini (texting) kama mbinu ya
mawasiliano. Waligundua kwamba, utumaji wa matini fupi fupi ni desturi inayokuwa haraka
hasa miongoni mwa vijana. Na kuwa kati ya Januari na Disemba 2000 matini fupi fupi (SMS)
zilizotumwa ziliongezeka kwa haraka kutoka matini bilioni nne na kufikia bilioni kumi na
tano kwa mwezi. Waliona kuwa matini kama hizo zitakuwa zimeongezeka na kuwa bilioni
200 kwa mwaka ifikapo Disemba 2001. Mtaalamu aliyeandika kuhusu aina ya ujumbe na
uundwaji wa lugha mpya ni Crystal (2008a; 2008b). Katika makala yake, aliyoiita Texting
(hapa ninaiita ‘Umatinishaji’), anasema kuwa umatinishaji ni jambo jipya kabisa ambalo sasa
linaelekea kupata lugha yake. Anaelezea kuwa katika umatinishaji, lugha mpya aliyoiita
textspeak inakua kwa haraka hasa miongoni mwa vijana. Makala yake hii ni ya msingi sana
katika mjadala wetu. Hata hivyo, makala ya Crystal iliongelea umatinishaji katika lugha moja
tu ya Kiingereza, na wala haikuonesha athari ya lugha hii “textspeak” au lugha tandawazi
katika nadharia za isimujamii.
Suala kubwa tunalolijadili katika makala hii ni changamoto zinazoletwa na lugha hii katika
Isimujamii, hasa kuchanganya msimbo (lugha) na kubadili misimbo (lugha) (code mixing and
code switching) au kama asemavyo King’ei “kuchanganya ndimi na kubadilisha ndimi”
(2010: 24). Tangu maandishi ya akina Blom na Gumperz (1972), suala hili la kuchanganya
msimbo na kubadili msimbo, limeshughulikiwa sana na wanaisimujamii. Waliolieleza kwa
kina ni pamoja na Labov (1973), Trudgill (2000), Meyerhoff (2006), na Nilep (2006) na hasa
zaidi utafiti na machapisho mbalimbali ya Myers-Scotton (1990, 1993a/1997, 1993b, 1993c,
2002). Hata hivyo, kwa wote hao ukimtoa Crystal (keshatajwa) hakuna aliyeshughulikia kwa
upana lugha ya simu za kiganjani; lugha ambayo hapa tumeiita ‘lugha tandawazi’.
Kwahiyo mwelekeo wa makala hii ni utafiti wa matumizi ya lugha hii tandawazi kwa
kuangalia simu za viganjani na athari yake katika nadharia za isimujamii. Madhumuni yetu ni
kuangalia matumizi ya lugha ya Kiswahili katika simu za viganjani. Kwa vyovyote vile,
matumizi ya Kiswahili cha leo katika simu yanafungua nafasi kwa matumizi ya lugha-pendwa
yanayosababishwa na utandawazi. Je Kiswahili cha kesho, tunaweza kubashiri
kitakavyokuwa na hivyo kukiandaa ili jamii ikipokee na kuendelea kukitumia? Ingawa
Crystal hadhani kuwa lugha hii ya simu itaathiri lugha ya kawaida ya Kiingereza,
inawezekana matokeo yakawa tofauti kwa lugha ya Kiswahili. Tukiangalia nyuma na kuitalii
historia ya makuzi ya lugha ya Kiswahili, tunaona kuwa Waswahili wa miaka iliyopita
walifanya kazi kubwa kukiandaa Kiswahili cha leo. Misingi iliyojengwa miaka ya nyuma
ndiyo iliyosimamisha nguzo za Kiswahili cha leo. Changamoto kubwa katika kukua kwa kasi
kwa lugha inaletwa na sayansi na matumizi ya teknolojia: vipengele viwili vinavyosukumwa
mbele na utandawazi. Kwahiyo, ili kujiandaa na ukuaji huo wa kasi, na ili tuweze kujua mwelekeo wa lugha na kuutawala, hatuna budi kuihakiki ‘lugha tandawazi’ kama hivi
vinavyoibuliwa leo na simu za kiganjani hasa miongoni mwa vijana. Tutafanya hivyo kwa
kuangalia mawasiliano miongoni mwa jamii za Tanzania tukijadili nafasi ya Kiswahili katika
mawasiliano hayo. Aidha tutaibua changamoto katika vipengele vya isimujamii ambapo
katika lugha tandawazi, tunaona upya unaotutaka tuziangalie tena tafsiri na maana ya kubadili
au kuchanganya msimbo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s