Mashairi bora ya Kiswahili.
UKIANGUKA MKUYU
Mama kumbi za sherehe,pindi tunapofurahi
Mama tupa starehe,atufanya twafurahi
Mama niwakusamehe,huwa mtu sahihi
Mkuyu ukianguka,wana wa ndege huyumba
Mama ndiye huwa duwa,pindi tuwapo mbali
Mama huwa muelewa,msimamo hubadili
Mama tukipitiliwa,mazito huyakabili
Mkuyu ukianguka,wana wa ndege huyumba
Mama ndiye letu jiko,pindi napohisi njaa
Mama ndo mshika mwiko,vyakula kuviandaa
Mama ndiye hangaiko,kutulisha atufaa
Mkuyu ukianguka,wana wa ndege huyumba
Mama ni hospitali,wagonjwa tunapokuwa
Mama ndo mwenye kujali,kwa kutupatia dawa
Mama huwa hawi mbali,tunapomhitaji huwa
Mkuyu ukianguka,wana wa ndege huyumba
Maadamu tuna mama,kwake sisi ni watoto
Tumpe zake heshima,sije katuchapa fito
Asije akalalama,sisi kwake ni uzito
Ukianguka mkuyu,wana wa ndege huyumba
(Malenga wa Nyali One-Agadias)