Mashairi aula ya Kiswahili.

SHAIRI: USINIHUKUMU
1.
Unionapo njiani, mikono narusharusha
Usicheke asilani, na ubaya kunivisha
Hulijui la moyoni, linalonihangaisha
Kamwe usinihukumu, nawe hutohukumiwa

2.
Usiniseme vibaya, kinyume ninapotenda
Usinione mbaya, ni dunia yaniponda
Yanisukuma pabaya, na maisha kunishinda
Kamwe usinihikumu nawe hutohukumiwa

3.
Vibaya nikiamua, usije kunihukumu
Nikichukua hatua, hatua iso muhimu
Usinihikumu pia, moyoni utie sumu
Kamwe usinihikumu nawe hutohukumiwa

4
Nina yanonisumbua, moyoni yanonitesa
Mawazo kunipatia, na furaha kuikosa
Mengi kuyakosea, kwa hali inonitesa
Kamwe usinihukumu, nawe hutohukumiwa

5.
Usije ukanikashifu, unionapo njiani
Useme ni mharifu, kunitia hatiani
Hakuna mkamilifu, Papa hapa duniani
Kamwe usinihikumu, nawe hutohukumiwa

6.
Usichambue zamani, zama ya maisha yangu
Wala usije tamani, kuijua zama yangu
Zamani iso thamani, ukaibua machungu
Kamwe usinihikumu, nawe hutohukumiwa

7.
Zama hii sitamani, mwenyewe kuikumbuka
Na machungu yanipeni, Kila napoikumbuka
Mawazo yanisongeni, mabaya kutendeka
Kamwe usinihikumu nawe hutohukumiwa

8.
Nimewatolea tusi, wasokuwa na hatia
Sababu yake ni hisi, hisia zilotokea
Hayajakuwa rahisi, maisha yanilemea
Kamwe usinihikumu nawe hutohukumiwa

9.
Usije uliza mbona, mbona sijafanya lile
Na kazini waniona, nang’ang’ana vile vile
Jua Nina nyingi Kona, ninaenda polepole
Kamwe usinihikumu, nawe hutohukumiwa

10.
Kiona nimenyamaza, na lolote sijasema
Jua mengi ninawaza, na mahali nimekwama
Dharau sijaikuza, ni mawazo sije lama
Kamwe usinihikumu, nawe hutohukumiwa

11.
Matambara nikivaa, sinicheke asilani
Kiatu kikichakaa, usinicheke asilani
Shida zimenifaa, zanipa umaskini
Kamwe usinihikumu, nawe hutohukumiwa

12.
Mwisho hapa ninakoma, kisema sinihukumu
Na kesho nitajituma, nami niwe wa muhimu
Ziniondoke lawama, waache kunilaumu
Kamwe Usinihikumu nawe hutohukumiwa

(MTUNZI:JUSTIN BIN ORENGE)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s