Mashairi Kuntu ya Kiswahili.
.DONGO
Dango – shabaha, lengo
Dingo – Aina ya mdudu
Wakongo – wagonjwa
Tengo – chengo, aina ya samaki
Mongo – mgongo
Banango – uharibikaji
Ngongongo – Tanakali ya sauti ya kitu kinachogongwa
Narusha dongo kwa dango, dingo lisende majongo
Lengo naliwe mpango, nisambe usongombwingo
Namwamba mwendo kibyongo, mwenye khuluka ya ungo
Dukale lifingwe fingo, asali sipigwe zongo
Ayasitiri maungo, pamwe ulivyo ubongo
Sehemu zilizo pango, ziwe ndani ya kifungo
Atahadhari na mwengo, mingi inayo matongo
Dukale lifingwe fingo, asali sipigwe zongo
Duniya ni mviringo, ya panda shuka viwango
Imesheheni waongo, na wa vimbwanga vibwengo
Asikuzuge utingo, wasafiri ni wakongo
Duka kalifinge fingo, asali sipigwe zongo
Matoyo yafanye tongo, utague kwa maringo
Uonapo ni mlango, katu si subiri hongo
Polepole kama bungo, nenda ukapike tengo
Duka ulifinge fingo, Asali sipigwe zongo
Tutagueni mipingo, ya kuyalinda matango
Yawekeke kicho chongo, huku twalinda kwa gongo
Silete mti sifongo, wakuyafyonza mafyongo
Maduka yafingwe fingo, asali sipigwe zongo
Tusingie kwa ulingo, mwilini tuwazi Mongo
Yajuweni masimango, ndicho chanzo cha borongo
Kisha tuje tungwa tungo, zichangiazo banango
Maduka yafingwe fingo asali sipigwe zongo
Wazazi chungeni chungo, kutwa muligadi jengo
Duka la vingi viungo, thamaniye ni mpingo
Mukililinda kwa lengo, zitakimbiya ngongongo
Maduka yafingwe fingo, asali sipigwe zongo
Yamejaa yenye nyongo, maduka ya mafinyango
Ya leseni za uongo, ziso vitwa wala shingo
Ndiyo yaletayo shango, kwa shahawa za mitwango
Maduka yafingwe fingo, asali sipigwe zongo
Nenda mkanga kaango, mekwisha timia mwongo
Nimeshaliranga rango, litekelezeni pungo
Penye na taka mapengo nimesha msinga singo
Maduka yafingwe fingo, asali sipigwe zongo.