Umalenga ni basi.

UMALENGA NI BASI
Moyo wangu umegoma, kutunga tena sidhani
Ushairi nauhama, malenga sina thamani
Bongo nalo limekwama, tungo hawazitamani
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Yani kote makundini, tungo zangu hazisomwi
Hata kule ulingoni, japo ya mbwa siamwi
Kule kwetu kisimani, naliwa na langu zimwi
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Mzee mpenda watu, hanioni mie kwani
Nazimaliza sapatu, kumfata kikashani
Kwake sisikiki katu, hanipi ‘ta tumaini
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Yule mhindi wa pwani, makundini simuoni
Hivi yuwapi jamani, Raneti aniauni
Azitupe ‘ko hewani, nisikike redioni
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Wenzangu magazetini, tungo zao zapepea
Taifa leo nyumbani, kila wiki watokea
Mwatumia mbinu gani, tungo zenu kutokea
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Huku wengine diwani, tungo zao zachapishwa
Kina Nuhu runingani, wanatamba bila rushwa
Navuma mitandaoni, vimoji vyarushwarushwa
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Pengine mnipe mada, niwaandikie wenza
Nisijezipata shida, mie bado najifunza
Nyumbani ninao muda, hivi kipi chaniponza
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Kama mie nina hila, nifunzeni si mjuzi
Au kama ni Kabila, siwezi pinga Mwenyezi
Kuwalipa sina hela, nawambia waziwazi
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki

Nawaaga kwaherini, nimechoka kulalama
Najitupa muzikini, nikazicheze ‘zo ngoma
Nitatoka makundini, msiambe sijasema
Naitupa mishororo, bora nifanye muziki.

(Daniel Wambua-Malenga)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s