Kauli yangu.

KAULI YANGU
Nawajia enyi wenza, watunzi mlobobea
Nahitaji kujifunza, tena nimejitolea
Zamani nyi mloanza, maswali nawaletea
Vipi nitakamilika, kwenye tungo kutajika?

Ningali nahanyahanya, wala sijakamilika
Hivi kipi sijafanya, ili nami kusikika
Nimejua mie panya, bado wapo wale paka
Mkishaondoka paka, mnijuze nitawale

Mrithi wenu ni papo, ‘Mola kinipa uhai
Niongoze hili jopo, sitokuwa mlaghai
Tusiweni kama popo, semeni kama sifai
Pale unaponisifu, siache kinikosoa

Kama kuna mitihani, basi mie sijapewa
Nawaomba watahini, kwenu nisijechelewa
Nisijeachwa gizani, vyeti kule wakapewa
Kama kunayo shahada, vipi nitaifikia?

Pia kama ni milango, basi leo naibisha
Kuchangizana kichango, mwalimu kanifundisha
Kengeza siiti chongo, ujumbe naufikisha
Kama bado kuna mwanya, naomba kuziba pengo

Walikuwepo zamani, washairi watajika
Yani kote duniani, hao ndo walosifika
Wakarudi kwa Manani, nanyi hapo mkafika
Pengine wakati wangu, ndo bado haujafika

Ndoto sitoivuruga, kuhamia muzikini
Naivunjaje miviga, kisa heti midundoni
Kamwe sitojikoroga, kujitoma tarabuni
Ushairi siuachi, mana ndo kipaji changu

Hata msipoyasoma, yananipa burudani
Miswada sitoichoma, kisa heti mwafulani
Lengo langu chanda chema, nivishiwe makundini
Ashakumu si matusi, msije kunifokea.

(Daniel Wambua-Malenga)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s