Zamani jama zamani.
ZAMANI
Nami leo nakumbuka,enzi zile kiwa kinda
Kwenu nyie nafunguka, ya utoto nilotenda
Wazazi walisumbuka, nilikuwa nimevunda
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Soka la makaratasi, lisoisha bila vita
Ngumi ningeziasisi, na matusi kuyabwata
Nikipigwa ni kisasi, sikubali katakata
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Ningatengeza manati, si ya shore wala mbuni
Nikuyagonga mabati, kisha paka wa jirani
Tena silivai shati, usiku hawanioni
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Usiku kwangu mchana, najitoma tarabuni
Na mbuga nilizichana, mama ajuwa ni ndani
Nirudi usiku sana, asubuhi ni chumbani
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Nachapwa nende chuoni, mwanawe nisome dini
Nikatoroke njiani, nende zangu mikanjuni
Kikoto kwani ni nini, siogopi abadani
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Shuleni nilibughudhi, kila siku ni adhabu
Walimu niliwaudhi, darasani nina tabu
Katu sikuwa na hadhi, nilizifeli hesabu
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Tungenda shule jirani, magongo ningeyabeba
Nikiyakumbuka Dani, sitamani kuwa baba
Midundo mingi garini, ya Matonya naye Kiba
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua
Niligomea chakula, nikakimwaga jikoni
Na wangu vibarakala, tukafukuzwa shuleni
Yakanitoka mashalla, utoto siutamani
Zamani jama zamani, wengine tulisumbua.
(Mtunzi:Daniel Wambua)