Nakupenda sio siri.
NAKUPENDA
Nikikutazama Dani, maneno hunikauka
Na moyo hukutamani, hisia ukaziteka
Naituma hino fani, kwako wewe itafika
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Natamani uwe wangu, mwamvuli kwayo mvua
Ni wewe chaguo langu, kivuli kwa lile jua
Nipo wazi si majungu, akili waizuzua
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Bora nifanye mtumwa, mtumwa wa huba lako
Siyafati yalosemwa, nawazia kuwa wako
Kwengineko nilitemwa, niweke moyoni mwako
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Bila wewe maishani, nitaikosa amani
Nakuahidi thamani, thamani iso kifani
Nitakuweka moyoni, naomba uwe mwendani
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Walisema ni safari, naomba kuanza nawe
Niishi nawe dahari, mauti yatuchukuwe
Mwana litie muhuri, nikupendae ni wewe
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Si lazima nioteshwe, ubavu wangu ni wewe
Au cheo nipandishwe, bora penzilo nipewe
Hata koo ikaushwe, ujumbe ni wako wewe
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Hata japo sina pesa, nina mapenzi ya dhati
Kwanini unanitesa, waniacha hatihati
Kila ninapopepesa, nakuona baidhati
Nakupenda sio siri, nimeshindwa kuthibiti
Naomba tuwe mapacha, mahabuba tufanane
Penzi letu ‘talificha, mahasidi wasilone
Nimeshindwa kulificha, nakomea hapa nane
Nakupenda sio siri, naomba unisitiri.
(Malenga ni Daniel Wambua)