Natamani.
NATAMANI
Walaiti ningakuwa, ja Stefano nipigwe
Mauti kunichukuwa, mie mfano niigwe
Kumbukumbu itakuwa, wasomaji msizugwe
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Nami niwe vitabuni, wanisome wasomao
Makala magazetini, wachapishe wawezao
Redio na runingani, watangaze wawezao
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Mitandao itingike, tungo zangu zimwagike
Wafikao nawafike, matozi yawamwaike
Na picha wazitundike, wengine wasikitike
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Nawaza kuwa waridi, niandikayo yapendwe
Wengine wasinirudi, kunichukia washindwe
Niwe mti wa baridi,popote pale nipandwe
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Nivikwe sifa sufufu, na wakubwa kwa wadogo
Wengi waje kunishufu, watambue mie mbogo
Wayasahau machafu, mwanya usiwe mdogo
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Wanikumbuke dahari, kizazi hadi kizazi
Kwingine niwe fahari, maishani niwe kwezi
Maneno yenye uturi, yani kama mtetezi
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Wakilisoma shairi, watamani kuniona
Maneno yangu mazuri, yasijeng’olewa shina
Wanisifu kwa uzuri, japo mie sipo tena
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe
Vyuoni hata shuleni, wanafunzi watahini
Wote wawe furahani, wakisoma zangu fani
Niwe mja wa thamani, nitambuke duniani
Natamani ningakufa, ja wengine nikumbukwe.
(Malenga ni Daniel Wambua)