Kwaheri Maradona.
KWAHERI DIEGO MARADONA
Wanasoka wanalia, huzuni umewafika
Zimewabana hisia, Maradona katoweka
Nyoyoni wanaumia, machozi yabubujika
Nenda vyema Maradona, daima utakumbukwa
Pengo lako kubwa mno, halizibiki daima
Uliyafanya manono, machache nitayasema
Hata japo kwa sonono, nitajikaza mtima
Nenda vyema Maradona, daima utakumbukwa
Twakumbuka pale Boka, hadi kule Barcelona
Nyavu zilivyotukuka, wenye macho waliona
Kiungo ulisifika, kwa soka Argentina
Nenda vyema Maradona, daima utakumbukwa
Ulivyofunga magoli, ilikujuwa dunia
Ulipofika Napoli, mabeki waliumia
Sevilla hadi Newelli, nani angekuzuia
Nenda vyema Maradona, daima utakumbukwa
Lile la mkono goli, wakauita wa mungu
Ukaitwaa medali, tena bila wanguwangu
Wakakuita fahali, sifa ziso na majungu
Nenda vyema Maradona, daima utakumbukwa
Zile zako rembaremba, kwalo guu la kushoto
Themanini ulitamba, hivi leo ni mapito
Kikosi kilijigamba, walijuwa wana moto
Nenda vyema Maradona, daima utakumbukwa
Lolote lenye na mwanzo, nao mwisho halikosi
Moyo wako ndio chanzo, poleni akina Messi
Alokuwa kama nyenzo, ugani yule farisi
Kalale mahala pema, Diego De Maradona.
(Malenga ni Daniel Wambua)