Zitaisha.
ZITAISHA
Lingawika lisiwike, kutakucha kulichele
Miale inimulike, nitachacha kwa kelele
Mato yangu yafunguke, ‘kifikicha kwa vidole
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Iniondoke senene, nizinduke niamke
Makomavu na manene, niyashike yashikike
Nilifikaje kwa nne, kwingineko nisifike
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Yangakuwa ni makali, ja usena wao nyuki
Yanitome wangu mwili, nitanena bila chuki
Yangawa kama sahili, nitaguna pasi haki
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Nyasi zile hunyauka, kiangazi kingatanda
Majani hupukutika, ardhini yakavunda
Nayo mvua ingafika, rangiye ungaipenda
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Naamini zimo njiti, si lazima kipekechwe
Ki pomoni kiberiti, bora jua lisikuchwe
Sitingiki kwa kijiti, vipi pembeni niachwe
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Masaibu yangazidi, kitwani ningayachuja
Yanganitia baridi, ningayapanga kwa hoja
Kamwe sitotaradadi, mambo kuyafujafuja
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Mawinguni kungatanda, kungaifunika anga
Kingavishwa pete chanda, ungalowa na mchanga
Yangaota nilopanda, unyunyu ningaupunga
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya
Micheye ingachepuka, rangi nzuri kukoleza
Kama chemi kulipuka, na uvundo ungaoza
Maji yangamiminika, chakacha ningazicheza
Zingakuwa nyingi dhiki, zitaisha siku moya.
(Malenga ni Daniel Wambua)