Natafutia wanangu.

NATAFUTIA WANANGU
Mimi yangu yameisha, langu lanipa kisogo
Nasubiria muosha, anioshe kama gogo
Wangu walinivukisha, nikavuka pasi zogo
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Nazifanya za sulubu, mavazi yamecharara
Kwingine niwe bawabu, kamwe halitonikera
Nitazamako ghaibu, japo ningali kapera
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Lau nitatunukiwa, hili ganda kugandua
Nami wana nikapewa, katu sitowagofua
Lishe bora watapawa, hata japo si halua
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Leo yangu naipanga, ya kesho hino safari
Nisije kuhangahanga, niwazie itibari
Nyumba leo naijenga, ili waje jisitiri
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Jasho lingabubujika, ninganuka kama vundo
Ngozi ikakunyanzika, shime nitakaza mwendo
Kamwe sitopumzika, ningakikosa kipando
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Waje wale kivulini, mie nilichotafuta
Papendeze baitini, uhawinde kufufuta
Kwao niwe na thamani, nyendo zangu kuzifata
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Nagaa gaa na upwa, kwa mpini nachanika
Ili wanangu na wapwa, kesho wasijeteseka
Wasile vilivyo chapwa, kwa waja wakawacheka
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu

Wasijekuwa mifano, ya watu waliokosa
Iwalegee mikono, kama wameitungasa
Kalamu yagoma wino, na maneno yamepusa
Dhiki ninazopitia, natafutia wanangu.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s