Walaji viporo.

Wale wapasha viporo, tabia hiyo acheni /
Mwaileta migogoro, hata haya hamuoni /
Na zote zake kasoro, mnatupia kinywani /
Viporo vina madhara, bure mwazichuma dhambi ////
*
Chakula umeshapika, kizuri tena cha moto /
Waanza kuyayatika, na kiporo kiso joto /
Sijui kipi wataka, zote hizi changamoto /
Viporo vina madhara, hata viliwe kwa ndimu ////
*
Waona unafaidi, ukila kwa kujificha /
Wafurahi maridadi, hukiogopi kuchacha /
Wakiona ni sitadi, ingali ulikiwacha /
Kiporo kina madhara, hata ukile gizani ////
*
Ulikiacha mwanzoni, ukenda pata cha moto /
Wakikumbukia nini, kiporo na hili joto /
Sendekeze fuadani, takuletea mazito /
Kiporo kina madhara, hata ukipashe moto ////
*
Kula hicho kilo moto, fureshi ulochagua /
Ukakiona fumbato, ndani ukenda kitia /
Yasikuhadae mato, kiporo kukumbushia /
Kiporo kina madhara, duniani na mbinguni ////
*
Uchumi unadorora, wahudumia viporo /
Nyumbani watia fora, huachi toa kasoro /
Wakacha maisha bora, menogewa na viporo /
Viporo vina madhara, hata ule kwa upole ////
*
Viporo vina madhara, akhera na duniani /
Vyaweza kupa kuhara, gonjwa la kinywa na chini /
Afyayo kudorora, ukabaki majutoni /
Viporo vina madhara, ukinaswa utajua ////
*
Hukilagi peke yako, wewe ulaye kiporo /
Jua yupo na mwenzako, nyote mwapigishwa doro /
Wewe watoa mshiko, yule juu ya godoro /
Viporo vina madhara, risechi yatuambia ////
*
Sicho cha halali kwako, wakila kwa kichochoro /
Huthamini afya yako, wauthamini mchoro /
Kutimiza haja zako, njaa gani ya kiporo /
Kiporo kina madhara, hata kifishwe uturi ////
*
Haimpendezi Mola, kurudia matapishi /
Waona raha kukila, waendelea kuishi /
Ipo siku atafula, kuujutia utashi /
Viporo vina madhara, havifai kurudiwa ////
*
Apime ayapimae, masafa niambaaye /
Kupinga anipingae, kiporo akisifiye /
Uzuriwe atugee, kiporo abugiaye /
Kiporo kina madhara, hata kiwe na chachandu ////

(Malenga ni Bin Omary)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s